Wanajeshi Mali wachukua nchi
BAMAKO,Mali
WANAJESHI walioasi nchini Mali wametangaza kwamba wamechukua udhibiti wa nchi ikiwa ni saa kadha baada ya kuvamia kasri ya rais.
Habari kutoka nchini humo zinaeleza kwamba wanajeshi hao walitoa tangazo hilo mapema jana huku wakipiga marufuku mtu yoyote kutoka nje nchi nzima na kwamba katiba haitatumika kwa sasa.
Kwa mujibu wataarifa hizo mapema juzi, wanajeshi hao walifyatuliana risasi na wanajeshi watiifu kwa serikali,wakisema kuwa serikali haijawapa silaha za kutosha kukabiliana na waasi wa jamii ya Tuareg.
Tayari walikuwa wamechukua udhibiti wa kituo cha taifa cha redio na televisheni na kusitisha matangazo.
Baada ya saa kadhaa ya kuonesha picha za nyimbo za wanamuziki wa Mali, kundi la wanajeshi likaonekana kwenye televisheni mapema jana wakitambulishwa kama "Kamati itakayorudisha Demokrasia na kutuliza hali katika nchi".
Msemaji wa waasi hao, aliyetajwa kwa jina la Luteni Amadou Konare, alisema sasa wamemaliza "utawala usio thabiti" wa Rais Amadou Toumani Toure
"Sisi walinzi wa Jamhuri na watu wake, tumelazimika kuchukuwa madaraka kutoka utawala ulioshindwa wa Amadou Toumani Toure na tutayakabidhi madaraka hayo kwa serikali itakayochaguliwa kidemokrasia." alisema Luteni Konare.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, wanajeshi hao sasa wameunda chombo walichokiita Kamati ya Kitaifa ya Kurudisha Utawala wa Kidemokrasia baada ya kuwatia nguvuni mawaziri kadhaa wa serikali ya Rais Toure.
Mwanajeshi mmoja aliliambia Shirika la Habari la Ufaransa AFP kwamba, miongoni mwa walio chini ya ulinzi ni Waziri wa Mambo ya Nje, Bw.Soumeylou Boubeye Maiga, na Waziri wa Mambo ya Ndani, Bw.Kafouhouna Kone.
Chanzo huru cha habari kilisema kwamba Rais Toure mwenyewe, ambaye mwanzoni walikuwa amezingirwa ndani ya kasri yake, alifanikiwa kuondoka eneo hilo salama na bado haijulikani alipo rais huyo, ambaye mwenyewe aliingia madarakani kwa mara ya kwanza kupitia mapinduzi ya kijeshi mwaka 1991.
Mapema nyakati za alfajiri kwa saa za Afrika ya Magharibi, milio ya silaha nzito na bunduki ilisikikana karibu na kasri hiyo na katika mji mkuu, Bamako, lakini mapambano hayo hayakuchukuwa muda mrefu wala hakujapatikana ripoti za maafa yake hadi sasa.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,(UN) Bw. Ban Ki-moon, ametaka kuwepo kwa hali ya utulivu na mazungumzo ya kutatua tafauti zilizopo kidemokrasia.
Ufaransa imewataka raia wa Mali kuheshimu utawala wa kikatiba na imelaani aina yoyote ya vurugu. Hata hivyo, haikusema ikiwa haiutambui utawala mpya wa kijeshi, badala yake mkoloni huyo wa zamani ametaka uitishwe uchaguzi "haraka iwezekanavyo."
Hivi punde, Jumuiya ya Uchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS) imepinga hatua hiyo ya wanajeshi kuchukuwa madaraka kwa nguvu.
"ECOWAS inalaani matendo haya yasiyo maana ya wanajeshi walioasi na inaonya kuwa haitavumilia kwa namna yoyote ile matumizi ya nguvu kama njia ya kutatua matatizo". ilieleza Jumuiya hiyo katika taarifa yake iliyotolewa mjini Lagos, Nigeria.(Reuters/AFP).
No comments:
Post a Comment